Latest News 13 Aug 2022

News Images

GAS ENTEC YATAKIWA KUONGEZA BIDII UJENZI WA MV MWANZA

Kampuni ya Gas Entec kutoka nchini Korea iliyopewa kandarasi ya ujenzi wa meli ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu imetakiwa kuongeza bidii ya ujenzi wa meli hiyo ili kuweza kukamilisha kwa wakati.

Hayo yamesisitizwa mapema wiki hii na Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Miradi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL). Lt.Col Mhandisi Revocatus Ntare wakati alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa meli hiyo katika bandari ya Mwanza Kusini, Mkoani Mwanza.

Akisisitiza suala hiyo Mha. Ntare alisema kuwa hali ilivyokuwa mara ya mwisho kamati hiyo ilipofika kwenye mradi ni tofauti na hali ilivyo kwani kuna hatua kubwa imepigwa katika ujenzi wa meli hiyo.

“Mwezi wa kumi mnaiweka kwenye maji lakini mwezi Mei iwe tayari imekabidhiwa kwa ajili ya kuanza operesheni za kusafirisha abiria kwenda sehemiu mbalimbali kama ilivyokuwa imepangiwa, kwa hiyo muweke bidii kama mlivyotuambia kwamba kazi zilizobaki humo ndani ni kufunga mambpo ya ‘Accomodation’ (malazi) na kwenye mainjini kule, muongeze bidii,” Alisema.

Aidha, alishauri kuwa baadhi ya maeneo ya ujenzi wa ndani ya meli hiyo ziweze kufanyika usiku na mchana ili watanzania waweze kuiona meli hiyo ikiwa kwenye maji tayari kwa kuanza kutoa huduma.

“Sasa hivi baadhi wanaona wanasema aah sasa mbona hamuanzi kusafirisha abiria, wakiona hivyo wanajua meli imekamilika, lakini najua kwa ‘speed’ (kasi) mliyonayo baada ya muda itakwenda vizuri, itapakwa rangi na kila kitu kitakamilika, na serikali itaona mnafanya kazi nzuri kwaajili ya watanzania,” Alimalizia.

Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji ndg. Philemon Bagambilana aliwashukuru Makandarasi hao baada ya kuona maendeleo makubwa ndani ya muda mfupi na kuwataka wasipunguze kasi hiyo ili watanzania waone chombo hicho kwenye maji.

“Safari hii tumeona maendeleo makubwa sana na kujituma kwingi, taswira ambayo hata wananchi ambao ndio walipa kodi, ambayo hiyo ndio imetumika kujenga hiki chombo wanapata matumaini, maendeleo ni makubwa na naomba hii speed (kasi) tunayokwenda nayo isipungue zaidi tu ya kuongezeka ili meli iingie majini mapema na wananchi waweze kupata chombo chao,” Alisema.

Hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai mradi huo umefikia asilimia 69 na mwezi Oktoba meli hiyo inatarajiwa kuingia majini.