Latest News 18 Jul 2024

MSCL YASHAURIWA KUITANGAZA MIRADI YA MELI KUKUZA UTALII NA UCHUMI WA BLUU
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Burundi Balozi Galius Byakanwa ameishauri Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kuona namna ya kuitangaza miradi ya ujenzi wa meli kwa wanafunzi na wazazi wasioifahamu tasnia hiyo ili waweze kujifunza fursa zinazopatikana katika uundwaji wa meli pamoja na ubaharia ili kukuza uelewa wa uchumi wa bluu nchini.
Balozi Byakanwa aliyasema hayo alipotembelea mradi wa Ujenzi wa Meli ya MV. Mwanza Hapa kazi Tu akiwaongoza wanafunzi 31 na waalimu wanne kutoka vyuo vikuu vya Jamhuri ya Burundi tarehe 13.07.2024 katika bandari ya Mwanza Kusini Jijini Mwanza.
“Tumekuwa na miradi ya kimaendeleo ambayo hatuioni kwa picha ya kiutalii, tunaiona meli inajengwa tu mwanzo mpaka mwisho lakini hatuoni kwamba kuna watu wanapaswa kuja wajifunze waone, lakini MSCL muichukue kama changamoto, msijenge meli tu ikamilike itoe huduma, mjenge meli iwe kivutio, waje waone meli inajengwaje na muonekano wake, kwahiyo hawa vijana wamekuja kwa kofia ya utalii kujifunza na kuona,” Alishauri.
Aidha, alieleza kuwa miongoni mwa sababu zilizowasukuma kufika kwenye mradi wa ujenzi wa meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu ni pamoja na kuitangaza Sera ya uchumi wa Bluu kimataifa ambayo ni sehemu ya Sera ya mambo ya Nje ya Tanzania.
“Hapa tulipo ni sehemu ya Uchumi wa Bluu. Meli hii itakuwa inasafiri kwa nchi zote za Afrika mashariki zinazotumia na Ziwa Victoria, jana tumeona daraja. Kwahiyo mrundi anayechukua bidhaa Kenya anaweza kuitumia hii meli kuchukua bidhaa kutoka Kisumu zinaletwa hapa zinapakizwa kwenye lori na kwenda Burundi,” Alisema.
Wakati akitoa taarifa ya mradi wa Ujenzi wa meli ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu Kaimu Mkurugenzi wa MSCL Wakili Alphonce Sebukoto alisema kuwa Mkandarasi anayejenga meli hiyo Gas Entec Ltd Kutoka Korea ya Kusini ameshalipwa asilimia 94 ya mradi na mradi upo katika asilimia 96.
“Tunasubiri wakamilishe kwa kufunga samani mbalimbali, meli hii itakapokamilika itakuguliwa na TASAC wanashughulika na kukagua usalama na kutoa cheti cha ubora ili iweze kufanya kazi,” Alisema.
Hata hivyo, Wakili Sebukoto alieleza mipango ya Serikali katika kuimarisha huduma za usafiri katika Ziwa Tanganyika ikiwemo kukarabati meli kongwe duniani ya MV. Liemba ambayo imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wanaofika nchini kutokana na historia yake na kuwa ni sehemu ya Urithi wa Taifa.
“Kutokana na matengenezo yatakayofanyika wakati wa utekelezaji wa mradi huu, meli ya MV. Liemba pindi itakapokamilika inatarajiwa kuhuishwa na kurejea katika hali yake ya upya na hivyo kuanza tena kutoa huduma ya usafiri kwa abiria na mizigo kwa wakazi waishio mwambao wa ziwa Tanganyika naukarabati wake unaanza mwezi huu wa Julai baada ya mkandarasi kulipwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.89,” Alisema.
Kwa upande wao wanafunzi walioshiriki kwenye ziara hiyo walifurahi kuona maendeleo yanayofanyika nchini Tanzania upande wa uchukuzi na kuahidi kuwa mabalozi wa kuwahamaisha wengine kufika nchini Tanzania ili kuweza kujifunza na kujionea maendeleo yaliyopo.
“Mimi kabla sijaja hapa kiutalii, sijawahi kuona meli kabisa, hivyo namshukuru Balozi wa Tanzania nchini Burundi kwa kutuleta ili tuweze kujionea wenyewe maendeleo yanayofanyika nchini Tanzania, kitu nilichojifunza ni kuina meli inayotengeneza kwa tecknolojia ya hali ya juu, wamesema ni meli ya kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa maziwa makuu hapa Afrika. Nitakwenda kuwaeleza wenzangu kule Burundi ili na wao waje kujionea na kujifunza,” Alisema Innocent Uwizeyimana, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Burundi.
Naye Asina Irakoze mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Burundi alifurahishwa kupata elimu ya uendeshaji wa meli na kufahamu kuwa meli haiendeshwi na mtu mmoja, hivyo inahitaji ushirikiano kuweza kuiongoza na kufika salama sehemu inapotarajiwa kufika.