Latest News 07 Sep 2022

News Images

MWENYEKITI WA BODI ATAKA UFANISI BAADA YA KUPOKEA MELI 3

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL) Meja Jenerali Mst. John Mbungo amewataka watumishi wa Kampuni hiyo kufanya kazi kwa ufanisi ili kuongeza pato la Kampuni pamoja na kukuza uchumi wa nchi.

Amesema kuwa Serikali imeonesha nia ya kuipa uwezo Kampuni hiyo kwa kuwakabidhi meli tatu zilizokuwa chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (TPA) ili kuweza kuziendesha hiyo ikiwa ni ukamilifu wa hatua mojawapo kati ya makubaliano kadhaa ikiwemo kukabidhi baadhi ya miundombinu inayoendana na utendaji kazi wa meli hizo.

“Wafanyakazi wa MSCL kwa kweli niwatake sasa wabadilike, kwa sababu Serikali inaonesha uwezo wake wa kuweza kufanya mabadiliko ndani ya Kampuni, kwahiyo sisi hatuwezi kubaki tena nyuma, lazima tubadilike, tufanye kazi kwa bidii, kwa maarifa na juhudi ili tuweze kuzalisha,” Alisema.

Hata hivyo, Meja Jenerali Mbungo alisisitiza kuwa watumishi wa MSCL hawana sababu ya kusuasua katika utendaji kazi na hivyo kuwaasa kutorudi nyuma na kuzisimamia vizuri meli hizo walizokabidhiwa.

Ameyasema hayo leo tarehe 07.09.2022 baada ya kutembelea meli tatu zilizokabidhiwa kwa MSCL pamoja na kuongea na watumishi wa Kampuni hiyo waliopo tawi la Kyela, Mkoani Mbeya katika bandari ya Itungi na Kiwira, Ziwa Nyasa.

Awali akitoa taarifa ya tawi hilo Kaimu Meneja Tawi wa MSCL Zacharia Mbilinyi alisema kuwa hivi sasa Kampuni hiyo inamiliki meli tano katika Ziwa Nyasa na idadi hiyo imeongezeka baada ya kukabidhiwa meli tatu kutoka TPA pamoja na meli mbili zilizokuwepo kabla ya kusimama kutoa huduma mwaka 2017.

“Meli hizi zinatoa huduma katika bandari 15 zilizoko katika mwambao wa Ziwa Nyasa katika Mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma ambapo kwa Mkoa wa Mbeya meli hizi zinatoa huduma katika bandari ya Itungi, Kiwira na Matema,” Alisema.

Meli za MSCL zilizokuwa zikitoa huduma katika Ziwa Nyasa ni MV. Songea yenye uwezo wa kubeba abiria 212 na tani 45.5 za mizigo pamoja na MV Iringa yenye uwezo wa kubeba abiria 139 na tani 5 za mizigo ambazo zilijengwa mwaka 1974.