Latest News 01 Jul 2022

News Images

RC Andengenye aahidi kufanya kazi na MSCL bega kwa bega.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kamishna Jenerali Mst. Thobias Andengenye ameahidi kutoa ushirikiano wa karibu katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inayofanyika katika bandari ya Kigoma, mkoani humo.

Mh. Andengenye amesema kuwa ushiriki wake katika kusimamia na miradi hiyo hahitaji kutengewa bajeti yoyote na MSCL na badala yake anahitaji kuarifiwa juu ya kinachoendelea na kutoa msaada pale inapobidi ili kusaidia kukamilisha utekelezaji wa miradi hiyo.

“Sisi na Marine Services Company Limited hatuhitaji bajeti kwaajili ya kwenda kufanya kazi, hata mafuta yakiisha hapa tunatembea kwa miguu, Mkitaka kunialika pale hamna ulazima wa kusema aah mimi sina bajeti ya kumuita Mkuu wa Mkoa aje aangalie, sihitaji bajeti yoyote nahitaji tu kuarifiwa kwamba bwana njoo kidogo utembee uje uone wala sihitaji chai wala zaidi ya kusaini kitabu cha wageni,” Alisema.

Aidha, aliwasihi viongozi wa MSCL kuhakikisha hawamsahau katika vichwa vyao na kumshirikisha kwa kila jambo linalotokea kwenye miradi na kusisitiza kuwa yupo pamoja kwenye safari ya kuhakikisha miradi hiyo inafanikiwa.

Mhe. Andengenye aliyasema hayo alipotembelewa na Uongozi wa MSCL ukiongozwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu Philemon Bagambilana pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi na Usimamizi wa miradi ya MSCL kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Luteni Kanali Revocatus Ntare wakati walipofika katika ofisi hiyo kwa nia ya kumjulisha uwepo wa kamati hiyo pamoja na kumpa taarifa fupi ya mradi unaoendelea pamoja na miradi inayotarajiwa kufanyika mkoani humo.

Wakati akitoa taarifa fupi ya mradi wa meli ya MT. Sanagara Bagambilana alisema kuwa mradi huo tayari umeshapokea awamu tatu za vifaa vya ukarabati wa meli hiyo na kutaraji kupokea awamu ya nne ya vifaa ifikapo katikati ya mwezi Julai, 2022 wakati mradi ukitarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2022.

Meli ya MT. Sangara inakarabatiwa na Mkandarasi KTMI Co. Ltd kutoka nchini Korea kwa thamani ya zaidi shilingi bilioni 8 na kutarajiwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2022.