Latest News 18 Jan 2023

News Images

Makubaliano ya CCTTFA na MSCL kuinua ufanisi sekta ya usafiri kwa njia ya maji

Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) na Wakla wa Uwezeshaji wa Usafiri wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) leo tarehe 17 Januari, 2023 zimesaini Makubaliano ya Ushirikiano (Memorandum of Understanding – MoU) yatakayodumu kwa muda wa miaka mitatu. Katika makubaliano hayo, CCTTFA itatoa uwezeshaji wenye thamani ya Dola za kimarekani 72,000 sawa na Shilingi 165,600,000/= kwa ajili ya kugharamia shughuli za utafiti wa masoko katika Ziwa Victoria na ZiwaTanganyika. Pia uwezeshaji huo utasaidia kugharamia zoezi la mapitio ya tozo za Kampuni kwa ajili ya kupata tozo mpya zinazoendana na hali ya soko kwa sasa.

Aidha uwezeshaji huo utasadia pia kuboresha eneo la mawasiliano ya MSCL ili kuongeza mwonekano wa Kampuni katika majukwaa mbalimbali ya kuuhabarisha umma ikiwemo, tovuti, mitandao ya kijamii, magazeti, Runinga, Radio pamoja na chaneli yetu ya YouTube inayojulikana kwa jina la “Meli TV”.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Katibu Mtendaji wa CCTTFA, Wakili Okandju Okonge Flory, aliahidi kuendeleza ushirikiano baina ya taasisi hizi kwa lengo la kuboresha huduma za usafirishaji kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika ambazo zinapakana na nchi za Ushoroba wa kati. “Katika kutekeleza mpango mkakati wa taasisi yetu, tuna wajibu wa kuchochea na kuendeleza usafirishaji wa majini kupitia maziwa yanayopakana nchi wanachama wa Ushoroba wa Kati ambayo ni Ziwa Viktoria na Ziwa Tanganyika na Kampuni ya Huduma za Meli ni mdau mkubwa kwenye kutimiza azma hiyo na nawaahidi tutaendeleza ushirikiano wetu kwani mafanikio yenu ni faida kubwa kwa wananchi wetu wa ukanda huu.” Alisema Wakili Okandju.

Makubaliano hayo ni muendelezo wa makubaliano ya awali baina ya taasisi hizi mbili ambayo yalisainiwa tarehe 16 Septemba, 2020 kwa ajili ya ufadhili wa kusomesha watumishi wa MSCL ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao. Ufadhili wa awali una thamani ya Shilingi 209,470,000/= na hivyo kufanya uwezeshaji wenye thamani ya Shilingi 375,070,000/= hadi sasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Eric Benedict Hamissi alieleza faida zilizotokana na makataba wa awali uliosainiwa mwezi Septemba, 2020 kuwa ni pamoja na kuhuisha vyeti vya mabaharia pamoja na kuwapatia mafunzo ya msingi ya ubaharia kwa watumishi ambao hawakupata mafunzo hayo.

“Kwa mkataba wa awali uliosainiwa mwezi Septemba,2020, watumishi wapatao 132 walifaidika katika maeneo tofauti ikiwemo kuhuisha vyeti vya ubaharia (revalidation),ili meli iweze kupata cheti cha ubora moja ya sifa ni kuwa na mabaharia wenye vyeti hai na hivyo kupitia fedha hizo MSCL iliweza kuhuisha vyeti vya mabaharia 49, na wengine waliweza kupata mafunzo ya msingi ya ubaharia (Mandatory course) pamoja na mafunzo ya usimamizi wa shughuli za usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya maji kwa wajumbe wa menejimenti ya MSCL.” Alifafanua Ndg. Eric Hamissi.

Kutokana na uwezeshaji unaoendelea kufanywa na CCTTFA kwa MSCL kupitia makubaliano yaliyosainiwa na pande zote mbili, MSCL inatarajia kuongeza ufanisi katika utendaji wake na hivyo kuwa na mchango chanya kwa utendaji mzima wa Ushoroba wa Kati.

CCTTFA ni taasisi ya kikanda inayoundwa na nchi tano ambazo Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ambapo makao makuu yako jijini Dar es Salaam.