Latest News 16 Apr 2024

News Images

TANZANIA KUWA KITOVU CHA UJENZI WA MELI NCHI ZA MAZIWA MAKUU

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizozungukwa na maji pande zote. Upande wa kaskazini, Ziwa Victoria, Kusini Mashariki, Ziwa Nyasa, Magharibi, Ziwa Tanganyika na Mashariki, Bahari ya Hindi. Si ajabu ikaitwa kisiwa cha amani kutokana na sifa hiyo.

Kwa kuiona fursa hiyo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kuzivuta karibu na bahari nchi zisizo na milango ya bahari zinazopakana na maziwa hayo makuu. Hayo yanadhihirika kwa kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji chini ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inayosimamiwa na Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa.

Baada ya Siku 34 tangu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 22 April 2021 alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jijini Dodoma na kueleza dhamira ya Serikali yake ya kuboresha huduma za usafiri kwa njia ya maji nchini

Siku hiyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema “Kwa upande wa usafiri wa majini, tutakamilisha ujenzi wa meli mpya na kuanza ukarabati wa meli ya mabehewa (yaani Ferry Wagon) kwenye Ziwa Victoria na pia kuikarabati meli ya MV. Liemba na kuanza ujenzi wa meli mpya kwenye Ziwa Tanganyika”.

Ziwa Victoria

Kwa mara ya kwanza nchi za Afrika mashariki na kati zimeshuhudia ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo ambayo kuanzia chuma cha kwanza cha mwili huo hadi kukamilika kwake imejengwa katika Bandari ya Mwanza Kusini Jijini Mwanza.

Meli hiyo yenye uzito wa tani 3500 itakayotoa huduma katika Ziwa Victoria imejegwa kwenye chelezo chenye uwezo wa kubeba meli yenye uzito wa hadi tani 4,000. Chelezo hicho pia kitatumika kujengea meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 na kukarabati meli ya mafuta ya MT. Nyangumi yenye uwezo wa kubeba lita 410,000 pamoja na kukarabati meli ya msaada ziwani ya MT. Ukerewe ambayo mikataba yake yenye gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni 160 imeshasainiwa.

Chelezo hicho hivi sasa kinatumika kukarabati meli za watu binafsi. Wajenzi pamoja na wamiliki wa meli Jijini Mwanza wamepongeza juhudi za Serikali za kuhakikisha huduma za usafiri kwa njia maji zinaimarika kwa Ziwa Victoria.

“Tunayo furaha kutumia hii chelezo muhimu, kubwa na ya kwanza kwa ukubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ni jambo zuri sana kwa MSCL kuwa na chelezo inayowawezesha wadau wa usafirishaji kupandisha na kushusha vyombo vyao kwaajili ya matengenezo na marekebisho.” Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Songoro Marine ndg. Major Songoro baada ya meli yao ya MV Rafiki 2 kushuka kwenye chelezo baada ya ukarabati mdogo.

Chelezo kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya meli mbili kwa wakati mmoja kutegemeana na ukubwa a meli hizo. Chelezo hiki kiligharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 36.4.

Ziwa Tanganyika

Tarehe 11.10.2023 Wananchi wa Mkoa wa Kigoma walishuhudia utiaji saini wa mkataba wa mradi wa ujenzi wa Karakana ya kujengea meli. Mradi huu haukuwahi kutokea katika nchi za Afrika hasa katika Ziwa Tanganyika linalounganisha nchi za Tanzania, DR Congo, Burundi na Zambia.

Uwekezaji unaofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wa zaidi ya Shilingi Bilioni 158 katika ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard), chenye uwezo wa kujengea meli kubwa zenye uzito wa hadi tani 5,000 katika Ziwa Tanganyika, unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika tasnia ya ujenzi wa meli nchini na ukanda wa nchi za maziwa makuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Ndg. Eric Hamissi alisema kuwa kiwanda hiki hakitatumika tu kujengea meli ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 bali pia kitakuwa ni muendelezo wa ujenzi wa meli nyingine kubwa ambazo zinatarajiwa kujengwa na taasisi yetu pamoja na waendeshaji wengine wa ndani na nje ya nchi.

“Kutokana na ukubwa wake, kiwanda hiki kina uwezo wa kuhudumia zaidi ya meli mbili kwa wakati mmoja kutegemeana na ukubwa wa meli hizo. Aidha, kiwanda hiki pia kitatumika kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa meli pindi inapohitajika kufanya hivyo na hivyo kutumika kama chanzo cha kuzalisha mapato kwa nchi,” Alisema Ndg. Eric Hamissi.

Wakati akihutubia katika hafla ya utiaji saini mkoani Kigoma, Mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mbarawa alisema kuwa Serikali imeamua kuwekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kujengea meli ili kuwezesha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo pamoja na miradi mingine iliyopangwa kutekelezwa siku za usoni.

“Itakumbukwa kwambaSerikali pia imepanga kujenga meli mpya ya kubeba abiria 600 na tani 400 za mizigo sambamba na kuzifanyia ukarabati meli za MV Liemba na MV Mwongozo. Hii inadhihirisha kwamba Serikali inatambua fursa kubwa za kimasoko zilizopo katika Ziwa hili kwa ajili ya kuhudumia wananchi wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa ambao wamekuwa na kiu ya muda mrefu ya kupata usafiri wa uhakika kwa njia ya maji kufuatia kuchakaa kwa meli zilizokuwepo na pia kusafirisha shehena nchi za jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia” Alifafanua.

Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 MSCL imesaini mikataba sita ya ukarabati na ujenzi wa meli. Miradi hiyo ni pamoja na Mkataba wa Ujenzi wa Kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika kwa gharama ya shilingi bilioni 303.5. Meli ya Mizigo Ziwa Tanganyika yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 kwa gharama ya shilingi bilioni 141.3 na meli ya mizigo Ziwa Victoria yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 kwa gharama ya shilingi shilingi bilioni 136.4.

Ukarabati wa meli ya MV. Liemba yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 200 za mizigo kwa gharama ya shilingi bilioni 32.9. Ukarabati wa meli ya kubeba shehena ya mafuta ya lita 400,000 iitwayo MT Nyangumi iliyoko Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 8.8 pamoja na Mkataba wa ukarabati mkubwa wa meli uokozi ya MT Ukerewe iliyoko Ziwa Victoria kwa gharama ya shilingi bilioni 6.3.