Latest News 16 Oct 2023
Zaidi ya bilioni 625 kujenga meli 2 mpya na kiwanda cha meli
Serikali kupitia Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) iliyo chini ya Wizara ya Uchukuzi imesaini mikataba mitatu ya ujenzi wa meli mpya mbili za mizigo na kiwanda cha kujenga Meli yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 625.
Hafla ya utiaji Saini wa mikataba hiyo ilifanyika mkoani Kigoma kati ya Serikali na kampuni ya Dearsan Shipyard ya Uturuki tarehe 11, Oktoba, 2023 na kushuhudiwa na mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa.
Kupitia mikataba hiyo, Serikali itajenga meli mbili mpya za mizigo zitakazotoa huduma Ziwa Tangayika na Ziwa Victoria.
Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Eric Hamissi amesema kuwa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha Meli utagharimu zaidi ya Sh322.7 bilioni na utakamilika ndani ya miezi 24 kuanzia mwaka wa fedha 2023/2024
Amesema mradi wa ujenzi wa meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 ya mizigo itakayotoa huduma Ziwa Tanzganyika utagharimu zaidi ya Sh158.27 bilioni na utekelezaji wake utakamilika ndani ya kipindi cha miezi 36.
‘’Meli hiyo itakuwa na uwezo wa kupakia malori marefu 25 au mabehewa 25 ya reli ya kisasa na magari madogo 65 itatumia muda wa saa sita kusafiri kutoka Bandari ya Kigoma hadi Bandari ya Kalemie nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),’’ amesema Hamis
Meli mpya ya mizigo itakayotoa huduma Ziwa Victoria ikiwa na uwezo wa kubeba tani 3,000 ya mizigo itajengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh145.4 bilioni na utakamilika ndani ya miezi 24 ya utekelezaji.
Akizungumzia miradi hiyo, Mhe. Mbarawa amesema utekelezaji wake unalenga kukuza biashara ndani na nje ya nchi kutokana na nafasi ya Tanzania Kijiografia katika Ukanda wa Maziwa Makuu.
“Kukamilika kwa miradi hii kutafungua fursa za kiuchumi, biashara na ajira kwa vijana,’’ amesema Mhe. Mbarawa
Kuhusu kiwanda cha kujenga meli ambacho ni cha kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Mhe. Mbarawa amesema kukamilika kwa mradi huo siyo tu kutawezesha Taifa kujitegemea katika shughuli za ujenzi wa meli, bali pia kutaokoa mamilioni ya fedha zinazotumika sasa kujenga meli nje ya nchi.
Mkurugenzi wa Huduma za Biashara ya Meli kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nelson Cosmas amesema shirika hilo la umma linashirikiana na taasisi zingine za Serikali kuhakiki michoro na kuipitisha.
‘’Tasac kwa kushirikiana na taasisi nyingine tuna jukumu la kusimamia hatua zote za ujenzi wa meli mpya na baadaye kusimamia uendeshwaji wake kwa mujibu wa sheria na kanuni za usafirishaji majini,’’ amesema Cosmas