Latest News 17 Feb 2023

News Images

MV. MWANZA ‘HAPA KAZI TU’ YASHUSHWA ZIWANI

Zoezi la kushusha meli ya MV. Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ limefanyikwa vyema kwa asilimia 100 huku ujenzi wake ukiwa umefikia asilimia 82.

Akizungumza Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi sekta ya Uchukuzi Mhe. Atupele Mwakibete kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Profesa Makame Mbarawa, wakati wa hafla ya ushushaji wa meli hiyo iliofanyika Bandari ya Mwanza Kusini, jijini Mwanza amesema kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), inatakiwa kuendelea kusimamia mradi wa ujenzi wa meli hiyo ili ukamilike ndani ya muda uliopangwa na kuanza kuwahudumia wananchi.

Pia amewataka kuhakikisha kuwa inasimamia miradi yote inayotekelezwa na Serikali kama ilivyopangwa ili kuleta thamani ya fedha iliyowekezwa.

Hata hivyo, ametoa rai kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuhakikisha inajipanga kuendelea kuboresha Bandari zilizopo Ziwa Victoria ili meli hiyo iweze kutia nanga bila shida wakati itakapoanza safari zake.

Mhe. Mwakibete ameeleza kuwa, Serikali imekuwa ikiwekeza kwenye miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na MSCL kwa lengo la kuboresha huduma ya usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya maji.

Amesema kuwa kujengewa kwa meli hiyo kutasaidia kufungua masoko mapya ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha safari mpya zitakazosaidia kurahisisha shughuli za kibiashara, kikazi, utalii na safari binafsi kwenye maeneo mengi zaidi ya ilivyo sasa.

“Meli hii itakapo kamilika ndani ya mwaka huu siyo tu kutakuwa na ongezeko la meli bali pia usafiri huu utakuwa umeboreshwa sana kwa vile meli itakuwa ya kisasa na yenye mwendo wa kasi zaidi ya meli zilizopo,”ameeleza Mhe. Mwakibete.

Sanjari na hayo Mhe. Mwakibete ameielekeza Menejimenti ya MSCL kubainisha vijana waliopata utaalamu kupitia mradi huo waweze kutumika kadri ya mahitaji ya Kampuni yatakavyojitokeza ili nguvu kazi yenye uzoefu isipotee.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Eric Hamissi,ameeleza kuwa meli hiyo itakapokamilika itahudumia bandari zote Kuu za Ziwa Victoria ikiwemo ya bandari ya Kemondo, Bukoba,Mwanza,Musoma na Portbell na Jinja za nchini Uganda pamoja na Kisumu nchini Kenya.

Ndg.Hamissi ameeleza kuwa meli hiyo ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu ina uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na magari makubwa matatu.

“Wakati Serikali ya awamu ya sita inapokea mradi huo ujenzi ulikuwa umefikia asilimia 45 laki mpaka leo inavyoshushwa ndani ya maji imefikia asilimia 82, huku Mkandarasi ameishalipwa asilimia 88 sawa na bilioni 93.8,” ameeleza Ndg.Hamissi.

Ameeleza kuwa meli hiyo itakuwa na madaraja sita ambayo ni VVIP itakayokuwa maalum kwa viongozi wa kitaifa ambapo watakuwa wanakaa watu wawili tu pamoja na viongozi wa kitaifa wa nchi jirani kama watapata kibali cha kusafiri na meli hiyo.

Huku ameeleza kuwa daraja la VIP ambalo litabeba watu mashuhuri sehemu hii itakuwa na watu wanne yaani vyumba vinne, daraja la kwanza litakalokuwa na watu 60, daraja la biashara litakalokuwa na watu 100 daraja la pili litakalokuwa na watu 200.

“Daraja la mwisho kwenye meli hii litakuwa ni la uchumi ambalo litakuwa linabeba abiria 834 na katika daraja hili kutakuwa na hadhi ya kisasa na wananchi watakaa kwa starehe na wataweza kufanya utalii,”amefafanua Ndg Hamissi.

Ndani ya meli hii pia kutakuwa na burudani,kutakuwa na sehemu ya ‘lift’ hasa kwa watu wenye changamoto ya kupanda ngazi na wagonjwa, na sehemu ya zahanati na sehemu ya wamama wajawazito

“Tunatarajia meli hii itakuwa inatumia masaa 10 pekee kwenda bandari ya Portbell nchini Uganda lakini pia itaenda Musoma mkoani Mara,” ameeleza Hamissi.

Meli hiyo inayojengwa na Mkandarasi GAS Entec kwa ushirikiano na Kagnam Corporation za nchini Korea pamoja na Suma JKT ya Tanzania itagharimu Shilingia Bilioni 109.15 hadi kukamilika kwake.