Latest News 04 Aug 2023

News Images

RAIS SAMIA AAHIDI KUWA WA KWANZA KUPANDA MV. MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa wa kwanza kuipanda Meli mpya ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu mara tu ujenzi wa meli hiyo utakapokamilika.

Aliyasema hayo Juni 14, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika Bandari ya Mwanza kusini alipofanya ziara ya ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa meli hiyo unaotekelezwa na Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Aidha, Rais Samia ameipongeza MSCL kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa meli hiyo ambayo imefikia asilimia 85 na hivyo kuelekeza kuendelea kuisimamia ili ikamilike kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa kimataifa.

“Niwashukuru sana mainjinia walioko hap ana wafanyakazi waliopo hapa, wakandarasi waliopo nawashukuru sana kazi zinakwenda vizuri, meli inakwenda kubeba abiria wengi 1,200 na tani 400 na hii ndio maana tuliyosema tunakwenda kuifungua Tanzania kiuchumi, kuwa na miundombinu ni jambo moja lakini kwa sisi watanzania kufanya kazi kwa bidi tukazalisha mashambani na viwandani ili bidhaa zetu zisafirishwe kwenda nchi Jirani ndio jambo la pili na ndio jambo kubwa,” Alisema.

“Nimeambiwa kuwa meli hii ndani ya kipindi kifupi itakuwa tayari, nataka niwaahidi ikiwa tayari nitakuwa wa kwanza kuja kupanda humu, nitaifungua mwenyewe nikiongozana nanyi wanamwanza tuingie humu tuzungushwe mpaka eneo fulani, kwasababu baada ya siku hiyo sidhani kama tutakuja kuipanda tena sisi wengine,” Alieleza.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MSCL Ndg. Eric Hamissi wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa meli ya MV. Mwanza hapa Kazi Tu alimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa pesa za kukamilisha mradi huo na kuahidi kuiendesha meli hiyo kwa manufaa kipindi itakapokamilika.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria ziara hiyo Mwanza Bi. Celina Joseph aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza miradi hiyo ambayo wananchi wengi walikuwa na dhana ya kuwa ingeendelea kusuasua.

“Kukamilika kwa mradi huu kutakua na manufaa sana kwa wakazi wa Mwanza na kuifanya Mwanza kua kitovu cha usafirishaji na kuongeza mzunguko wa fedha utakao fungua uchumi sio tu kwa kanda ya ziwa bali hata nchi jirani za Kenya na Uganda.”

Meli ya MV.Mwanza Hapa Kazi Tu itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kubwa ya kwanza ya abiria na mizigo kujengwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki yenye uwezo wa kubeba abiria 1200 na tani 400 za mizigo na inatarajia kuanza safari zake mwisho wa mwaka huu 2023.